Kama wewe ni mtumiaji wa programu mbalimbali basi lazima utakuwa unajua kuwa Dark Mode au muonekano mweusi ni sehemu ya muhimu sana kwenye programu za siku hizi. Sehemu hii huweka muonekano mweusi kwenye programu husika na kuondoa rangi nyeupe na hivyo kufanya macho ya mtumiaji kuwa salama hasa anapokuwa anatumia programu hiyo wakati wa usiku.
Sasa siku za karibuni tumeona jinsi ya kuwasha muonekano huo mweusi kwenye kompyuta za Windows na Mac, lakini pia kidogo tuliangalia jinsi ya kuwasha sehemu hiyo kupitia programu na tovuti ya Tanzania Tech.
Kama kwa namna yoyote ulipitwa na makala hiyo basi labda nikufahamishe kwa ufupi kuwa unaweza kuwasha dark mode kwenye app ya Tanzania Tech kwa kubofya kwenye sehemu ya Mpangilio > Kisha chagua Soma Usiku. Kwenye tovuti ya Tanzania Tech bofya alama ya mwezi iliyopo juu upande wa kulia.
Sasa tuki achana na muonekano wa giza wa Tanzania Tech, sasa unaweza kuwasha muonekano huu wa giza kwenye kila tovuti unayotembelea kupitia kivinjari cha Google Chrome kwa mfumo wa Android. Ili kuweza kuwasha sehemu hii kwa sasa itabidi kutumia njia ya Flags ambayo nitakuonyesha hapo chini. Kama hujui kuhusu Flags basi unaweza kuangalia video hapo chini ya mambo ambayo ulikuwa huyajui kuhusu Google Chrome.
Sasa kama video hiyo ilivyo elekeza, ili kuwasha muonekano huu mweusi ingia kwenye kivinjari chako kisha bofya sehemu ya kuandika alafu andika chrome://flags.
Baada ya hapo utaona ukurasa mpya umefunguka wenye neno Experiments kwa chini. Kwenye sehemu ya kutafuta kwenye ukurasa huo (sehemu hiyo imeandikwa Search Flags) andika Dark Mode
Utaoa sehemu imeandikwa Android web contents dark mode, bofya kwenye sehemu iliyo andikwa Default kisha chagua Enabled.
Baada ya hapo bofya sehemu ya Relaunch itakayo tokea chini upande wa kulia. Baada ya hapo utaona kivinjari cha Chrome kimejifunga na kujifungua kisha ukingia kwenye sehemu ya kutafuta kitu mtandaoni utaona sasa ina muonekano wa rangi nyeusi.
Kama kwa namna yoyote hauto pendezwa na muonekano huo unaweza kurudia hatua hizo kisha bofya sehemu hiyo na weka default au unawea kubofya sehemu ya Reset all to default kisha funga kabisa kivinjari cha chrome na ufungue tena, sehemu hiyo kama inaonekana kwenye picha hapo chini ipo upande wa kulia juu.
Kama umefanikiwa kuwasha muonekano huo hebu tuambie maoni yako unaonaje muonekano huo na pia kama hujapenda muonekano huo unaweza pia kutuambia kupitia sehemu ya maoni hapo chini.