Benki ya CRDB imetoa zawadi kwa wanafunzi wa vyuo mbalimbali nchini ikiwa ni sehemu ya kampeni ya JIPE 5 ambayo ilizinduliwa mwezi Oktoba mwaka huu ikiwa na malengo ya kuhamasisha Watanzania kujiwekea akiba kuelekea mwisho wa mwaka.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Meneja Mwandamizi wa Idara ya Wateja Binafsi wa Benki ya CRDB, Abel Lasway amesema kuwa hadi kufikia tarehe 16 mwezi huu, benki tayari imeshatoa jumla ya zawadi zinazofikia Shilingi Mlioni 20. Zawadi hiyo zimetolewa kwa wateja zaidi ya 4000 huku akaunti zaidi ya 74,000 zikiwa zimekwisha funguliwa.
“Tunawashukuru sana Watanzania kwa kuipokea vyema kampeni ya Jipe Tano ambapo mafanikio yaliyopatikana sio tu ni kwa faida ya Benki ya CRDB bali yanaonyesha ni kwa jinsi gani Benki ya CRDB imeweza kuwajumuisha Watanzania wengi katika mfumo rasmi wa huduma za fedha,” alisema Lasway.
Meneja huyo mwandamizi alisema katika kampeni hiyo ya Jipe Tano makundi mbalimbali ya wateja yameweza kuzawadiwa ambapo kwa mwezi huu wa Disemba Benki inawazawadia ada za shule wazazi wanaofungua akaunti ya watoto za Junior Jumbo. Jumla ya Shilingi Milioni 30 zimeandaliwa kwa ajili ya kutolewa kama zawadi ya ada kwa akaunti za watoto za Junior Jumbo zitakazofunguliwa mwezi Disemba.
“Benki ya CRDB tunajinasibu kwa kauli mbiu yetu ya “Ulipo Tupo” ambayo haiishii tu kufikisha huduma mahali ambapo wateja wetu wapo bali inalenga kuhakikisha Benki inakua pamoja na mteja katika hatua zote za maisha yake,” aliongezea Lasway.
Sambamba na zawadi hizo kwa akaunti za akiba na watoto, alisema Benki ya CRDB pia ililenga kundi la wanafunzi wa vyuo ambavyo vimefunguliwa hivi karibuni ambapo timu ya mauzo ya Benki iliweka kambi katika vyuo mbalimbali nchini ili kutoa elimu ya masuala ya fedha pamoja na kutoa huduma za kufungua akaunti kwa wanafunzi.
“Nimefurahi kuona tumeweza kufanikiwa kuwaingiza katika mfumo rasmi wa fedha wanafunzi wengi na tukaona pamoja na kuwapa huduma hizi tuweze kuwazawadia vitu ambavyo vitarahisha maisha yao wawapo chuoni,” alisema Lasway huku akiongeza kuwa kupitia kampeni hiyo ya wanafunzi ya JIPE 5 na Scholar, jumla ya wanafunzi 100 kutoka vyuo mbalimbali nchini watazawadiwa laptop (kompyuta pakato) na smartphone (simu janja).
Akizungumza baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa laptop (kompyuta pakato), Jackline Masayanyika mwanafunzi kutoka chuo cha Mtakatifu Agustino kilichopo jijini Mwanza, amesema kuwa zawadi hiyo itakua msaada mkubwa katika masomo yake ukizingatia uwepo wa fursa nyingi za masomo zinazopatikana mtandaoni