Kampuni za kutoa huduma za simu nchini China, hivi leo zimezindua rasmi huduma za mtandao wa 5G na kuanza kuhudumia wateja wake kwa kuwapa vifurushi vya 5G vya gharama nafuu. Kwa mujibu wa tovuti ya south china morning post, kampuni za simu za China Mobile, China Unicom, na China Telecom tayari zimeanza rasmi kutoa huduma hizo nchini humo.
Inasemekana kuwa kampuni hizo zimeanza kutoa vifurushi vya 5G kuanzia Yuan ya china CNY 128 ambayo ni sawa na takribani Shilingi za kitanzania TZS 42,000 kwa GB 30 za 5G hadi kufikia Yuan CNY 599 ambayo ni sawa na Shilingi za kitanzania TZS 197,000 kwa GB 300 za 5G.
Hata hivyo inasemekana kuwa vifurushi vya 4G havija pishana sana bei na vifurushi vya 5G hivyo mitandao hiyo inatoa huduma hizo za 5G kwa bei inayo fanana kabisa na vifurushi vingine.
Kutokana na kampuni hizo kubwa nchini humo kujiunga na mtandao wa 5G, Kwa sasa China inakuwa ndio nchi ya kwanza duniani kwa kuwa na mtandao mkubwa wa 5G kuliko nchi nyingine duniani. Hata hivyo kwa mujibu wa tovuti ya SCMP, Serikali inatarajia kwamba ifikapo mwaka 2020 zaidi ya watumiaji milioni 110 watakuwa wameingia kwenye mtandao mpya wa 5G nchini humo.
Kwa hapa Afrika bado kampuni mbalimbali zinaendelea kufanya makubaliano na kampuni ya Huawei kwa ajili ya kufunga vifaa maalum vya kuwezesha mtandao wa 5G, huku kwa sasa Afrika kusini ikiwa ndio nchini ya Kwanza hapa barani Afrika kuwa na mtandao wa 5G unao fanyakazi. Huduma hizo zinatolewa na kampuni ya simu ya Rain ambayo inatoa huduma hizo kwa baadhi ya sehemu kwenye mji wa Johannesburg na sehemu za karibu.