Mwanzoni mwa mwaka jana 2017, kampuni ya Blackberry ambayo inaendeshwa na kampuni ya TCL, ilitangaza ujio wa simu yake mpya ya Blackberry Motion, simu hii ilikuja na sifa kadhaa ambazo zinafanana na simu nyingi za Android za mwaka jana lakini pia muonekano wa simu hii ni sawa na muonekano wa simu nyingi za Android za mwaka 2017.
Mbali na muonekano wa simu hiyo, hivi karibuni wapenzi wa simu za Blackberry wa hapa Afrika, kwa mara ya kwanza wataweza kufurahia na kuimiliki simu hiyo kutoka kampuni ya Blackberry. Kwa mujibu wa taarifa kutoka tovuti ya Crack Berry, simu hii imeanza kupatikana rasmi hapa Afrika na kwa kuanza itaanza kupatikana rasmi nchini Afrika ya Kusini.
Simu hii itakuwa inapatikana kwa Rand ya Afrika Kusini R6,999 sawa na Shilingi za Tanzania Tsh 1,278,000, huku wateja wa Vodacom wa nchini humo wakipewa nafasi ya kumiliki simu hiyo kwa kuinunua kwa vifurushi kuanzia Rand R399 kwa mwezi sawa na Tsh 73,000 kwa mwezi.
Kwa sababu simu hii imeshafika Afrika Kusini ni wazi siku sio nyingi utaweza kuinunua kwenye maduka mbalimbali ya hapa Tanzania, bila shaka ikiwa pamoja na kwenye maduka ya Vodacom ya hapa Tanzania. Endelea kutembelea Tanzania Tech tutakujuza pindi simu hii itakapo anza kupatikana hapa nchini Tanzania.