Kwa muda sasa nimekuwa nikiwaza kuandika kuhusu biashara ya dropshipping lakini kutokana na kukosa ujuzi wa biashara hii basi ilinibidi kusoma zaidi kuhusu biashara hii ikiwa pamoja na kupata ujuzi wake kwanza kabla ya kuja kwenu.
Hadi sasa natumaini nimejifunza machache kuhusu dropshipping na sasa natumaini nipo tayari kuwa fahamisha yale machache niliyo yafahamu kuhusu biashara hii ya mtandaoni. Basi bila kupoteza muda twende nikufahamishe kuhusu haya machache.
TABLE OF CONTENTS
Nini Maana ya Dropshipping
Dropshipping ni biashara ya mtandaoni ambayo inahusisha soko la mtandaoni, biashara hii huweza kufanyika kwa mtu kuweza kuuza bidhaa mtandaoni bila kuwa na stock ya bidhaa unazoziuza.
Kuelewa zaidi, hii ni sawa na kusema Dropshipping ni kama biashara ya udalali yaani una msaidia mtu kuuza bidhaa yake na matokeo yake unaweza kupanga bei unayotaka na kumpa mwenye mali pesa anayohitaji na wewe kubaki na kiwango ulicho ongeza kwenye bei yako.
Kama unavyoweza kuona hapo juu, mfumo wa dropshipping unavyofanya kazi ni lazima kuwa na soko la mtandaoni kwani hapo ndio sehemu ambayo wateja wako hununua bidhaa zako.
Je Nani Anaweza Kufanya Dropshipping
Mtu yoyote mwenye uwezo wa kufungua tovuti ya kuuza bidhaa mtandaoni anaweza kufanya biashara ya dropshipping. Lakini ni vyema kufahamu kuwa biashara hii inaushindani mkubwa kutokana na kuwa na gharama nafuu za kuanza biashara hii hivyo watu wengi hufanya biashara hii.
Je Kuna Gharama Gani Kuanza Biashara Hii
Kwenye swali hili hakuna jibu la moja kwa moja kwani unaweza kuanza kwa kiwango kidogo hadi TZS 200,000 kwaajili ya kutengeneza soko la mtandaoni au zaidi ya hapo. Lakini ni vizuri kujua kuwa biashara hii imejikita zaidi kwenye matangazo hivyo ni vizuri kutenga kiasi fulani cha pesa kwaajili ya kufanya matangazo ili kujulisha wateja kuhusu soko lako.
Je Kuna Faida Gani Kuanza Biashara ya Dropshipping
Kama nilivyo kwambia hapo juu, biashara hii ni rahisi sana kuanza na kama ukifanya biashara hii kwa usahihi basi unaweza kupata faida sana hasa pale soko lako linapojulikana sana mtandaoni. Pia kutokana na kuwa huifadhi mizigo yoyote ya mteja basi unazidi kupata urahisi na faida kwa wingi. Pia unaweza kuuza bidhaa popote duniani bila kujali wewe ulipo.
Matatizo ya Biashara ya Dropshipping
Kila biashara ina faida na hasara, tofauti na biashara nyingine biashara ya dropshipping inaweza kuwa na kikwazo pale mteja wako anapo cheleweshewa kupata mzigo wake, au pale mteja anapo pokea oda ambayo sio sahihi. Hapa inakubidi wewe kuongea na msambazaji ili kuweza kumsaidia mteja. Mara nyingine inakubidi kurudisha pesa kwa mteja kama msambazaji wako hato toa ushirikiano na wewe.
Je Biashara ya Dropshipping ni Nzuri kwa Tanzania
Ukweli ni kwamba biashara yoyote ni nzuri kwa Tanzania tatizo ni aina ya wafanya biashara wa kitanzania. Hapa kwetu Tanzania watu wengi wanapenda kufanya biashara ili wafanikiwe haraka na hii imekuwa ni chanzo cha biashara nyingi za mtandaoni kushindwa kuendelea au kuwa na utapeli mwingi.
Hii imepelekea watanzania wengi kushindwa kutengeneza msingi (tovuti za kisasa) ambazo zina aminika na hivyo kushindwa kufanya biashara hii. Hivyo kama ukifanya biashara hii kwa uvumilivu na kwa uaminifu basi kwama wewe ni mtanzania utaweza kufanikiwa.
Je Unataka Kuanza Biashara ya Dropshipping
Kama unafikiria kuanza biashara ya dropshipping unaweza kuanza kwa kununua domain pamoja na hosting kisha tengeneza soko bora la mtandaoni. Muonekano ni muhimu kwa wateja wako hivyo hakikisha tovuti yako inaonekana vizuri kwani itasaidia kuweza kuaminika zaidi, pia unaweza kutengeneza apps za Android na iOS kwaajili ya kuvuta wateja zaidi kwani asilimia 80 ya matumizi ya Internet yanatoka kwenye simu za mkononi.
Na hayo ndio machache kuhusu dropshipping, kama unayo maswali au una maoni kuhusu makala hii unaweza kuuliza kupitia sehemu ya maoni hapo chini. Kwa makala zaidi kama hizi hakikisha unaendelea kutembelea Tanzania Tech kila siku.