Serikali ya India hivi leo imetangaza kufungia app ya TikTok na nyingine 58 ambazo zinasemekana kumilikiwa na kampuni mbalimbali za nchini China.
TikTok na app nyingine za China, zimekuwa zikipitia matatizo mengi kutokana na kile kinachosemekana kuwa apps hizo hazina usalama kwa asilimia 100. Hata hivyo, mbali na app ya TikTok apps nyingine maarufu ambazo zimezuiliwa nchini India ni pamoja na app ya Likee, UC Browser, Shareit, We Chat, Cam scanner na nyingine nyingi.
Kwa mujibu wa PIB au Press Information Bureau ya nchini India, sababu za kutoa apps hizo ni kutokana na kulinda masilahi ya watumiaji wa simu za kihindi na wavuti. “Uamuzi huu ni hatua inayolenga kuhakikisha usalama na uhuru wa watumiaji wa kihindi.” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa sasa bado tunaendelea kusubiri taarifa zaidi kuhusu ili, huku apps hizo zote zikiendelea kutokuwepo kwenye masoko ya Apps nchini India.
Hii sio mara ya kwanza kwa app ya Tik Tok na nyingine kutolewa kwenye soko la Play Store na App Store. Mwaka jana 2019, TikTok iliondolewa tena kwenye soko la Play Store kwa kile kilicho semekana kuwa app hiyo inasambaza video ambazo zipo kinyume na maadili. App ya Tik Tok inaongoza kwa kupakuliwa na watumiaji nchini India, huku asilimia zaidi ya 50 ya watumiaji wote wa app hiyo wakiwa ni watumiaji kutoka nchini humo.
Kwa sasa taarifa hii inaendelea hivyo tutaendelea kukuleta taarifa zaidi pale tutakapozipata, endelea kutembelea Tanzania Tech.