Mtandao maarufu kwa kuuza bidhaa mbalimbali wa AliExpress, hivi karibuni umekamilisha makubaliano na mtandao wa Safaricom nchini Kenya na hivi karibuni mtandao huo unategemewa kuanza kupokea malipo kwa M-Pesa.
Safaricom ambayo ni sawa na mtandao wa Vodacom Tanzania, umekuwa na juhudi binafsi za kuhakikisha manunuzi mtandaoni yanakuwa rahisi na kuwezesha watumiji wa mtandao huo kupata huduma za mtandao kwa urahisi zaidi. Siku za karibuni, mtandao huo uliwezesha huduma ya kuamisha pesa kutoa mtandao wa Paypal kwenda M-Pesa huduma ambayo kwa hapa Tanzania bado ni hadithi isiyokuwa na mwisho.
Mbali na hayo, huduma za M-Pesa kupitia mtandao huo wa Safaricom hivi karibuni ziliboreshwa na kuwekewa huduma mpya ya (Overdraft) ambapo mtumiaji anaweza kutumia zaidi ya kiwango alichonacho pale anapo lipia bidhaa kwa kutumia M-Pesa.
Kwa mujibu wa tovuti ya Business Day, Safaricom imekamilisha makubaliano hayo ikiwa kama hatua ya kampuni hiyo kufanya huduma za M-Pesa kuwa moja ya huduma itakayoweza kutumiwa na watu wote duniani kama njia ya malipo.
Kuwepo kwa huduma hii kutawezesha watumiaji wa mtandao huo nchini Kenya kununua bidhaa mbalimbali kupitia AliExpress bila kuwa na kadi ya benki au Credit Card. Tovuti ya AliExpress ni moja kati ya tovuti kubwa duniani za kununua bidhaa mbalimbali kutoka nchi mbalimbali ikiwa pamoja na China. AliExpress ni sehemu ya huduma zinazotolewa na kampuni ya Alibaba.
Safaricom ni mtandao unao ongoza nchini Kenya, huku ukisemekana kuwa na zaidi ya asilimia 65% ya watumiaji wa simu nchini Kenya, hii ini sawa na kusema mtandao huo una watumiaji milioni 30 nchini humo.