Hayo yamesemwa kupitia gazeti la mwananchi hivi karibuni baada ya mkurugenzi mtendaji wa Vodacom, Ian Ferrao kuulizwa kuhusu usalama wa fedha za wateja wa M-Pesa ambao kwa sababu moja au nyingine hawatumii akaunti zao kwa muda mrefu.
Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa “Akaunti huendelea kuwa hai kwa siku 270 baada ya hapo salio lililopo huhamishiwa Benki Kuu na akaunti kufungwa kwa mujibu wa sheria. Lakini endapo mteja atafanikiwa kujitokeza kwa muda, salio lake hurudishwa,” alisema Ferrao.
Habari hii imetoa mwanga kwa watu wengi sana ikiwemo mimi, kwa kujua kuwa kumbe kama akaunti ina hela na imekaa kwa muda mrefu bila kufanya miamala yoyote yaani ya kutoa au kuweka pesa basi akaunti hiyo inaweza kufutwa na pesa hizo kuchukuliwa na serikali. Sasa kupitia habari hii haya hapa ni mambo ya msingi ambayo tumeweza kugundua na ambayo tungependa na wewe uweze kuyafahamu.
- Kampuni za Simu Hazitunzi Fedha.
Hapa ni kuwa kumbe kampuni za simu hazi hifadhi pesa zako bali kinachotokea ni kuwa, Fedha zote za wateja zinahifadhiwa kwenye akaunti ya benki inayoitwa Trust. Hivyo basi Mteja ambaye hajatumia akaunti yake kwa muda mrefu, salio lake huhamishiwa Benki Kuu kwa mujibu wa (Sheria ya Mali Iliyosahaulika) au Unclaimed Property Act.
- Baadae Fedha Hizo Huhamishiwa Serikalini.
Hapa ni kuwa endapo mteja husika hatajitokeza kutumia akaunti yake kwa muda muafaka, basi fedha hizo huhamishiwa serikalini kama inavyoagizwa na utaratibu uliopo. Kwa upande wa mifumo ya malipo, hususan miamala ya fedha kwa njia ya simu, kifungu cha 31 cha Kanuni za Fedha za Miamala 2015 kifungu hicho husimamia utaratibu huo.
- Kigezo ni Ukomo wa Miaka Mitano Pasipo Mwenye Akaunti Kujitokeza.
Kwa mujibu wa kanuni hiyo hapo juu, kigezo kikubwa kinachozingatiwa kuifanya akaunti ionekane imetelekezwa ni ukomo wa miaka mitano pasipo mwenye akaunti kujitokeza. Baada ya muda huo kupita bila mwenye akaunti kujitokeza, Benki Kuu huziwasilisha fedha husika serikalini kupitia kwa Msajili wa Hazina baada ya kuzipokea kutoka kwa watoa huduma yaani makampuni ya simu. Hata hivyo endapo mteja wa akaunti hiyo atapatikana au mrithi wake akajitokeza, akikamilisha taratibu za mirathi, basi kampuni husika ya simu humsaidia kupata fedha zake.
- Mteja Asipojitokeza kwa Miaka 15 Serikali Huzitumia fedha Hizo
Kwa mujibu wa gazeti la mwananchi ambalo liliongea na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Benki na Taasisi za Fedha wa BoT, Kennedy Nyoni ambae alisema kuwa, utaratibu huu pia hutumika kwenye akaunti za benki za biashara ambapo mteja asiyeitumia fedha kwenye akaunti yake kwa muda wa miaka 15 mfululizo, salio lililopo huhamishiwa BoT na hii usababishwa na Sheria ya mali iliyotelekezwa au abandoned property ya Benki na Taasisi za Fedha.
Na hayo ndio mambo ya muhimu ambayo wewe kama mtumiaji wa mitandao hii ya simu ni vyema ungeyafahamu. Je wewe unaonaje kuhusu hili..? tuambie kwenye maoni hapo chini.
Kwa habari zaidi za teknolojia hakikisha una download App yetu mpya ya Tanzania Tech kupitia Play Store na vilevile tembelea channel yetu ya Tanzania Tech kupitia Youtube ili uweze kujifunza zaidi mambo yote ya teknolojia kwa njia ya Video.