Wakati jitihada za kuhamia kwenye mtandao wa 4G zikiendelea kwa baadhi ya makampuni ya simu hapa Tanzania, Afrika kusini imeingia kwenye historia kwa kuwa nchi ya kwanza kwa bara la Afrika kuwa na mtandao wenye kasi wa 5G.
Kwa mujibu wa tovuti ya Forbes, kampuni ya kutoa huduma za simu ya nchini humo inayoitwa Rain, ime fanikiwa kuwezesha mtandao wa 5G kwa matumizi kamili kuanzia mwezi huu. Kwa mujibu wa tovuti hiyo, inasemekana kuwa mtandao huo unategemewa kutumika kwanza kwenye mji mkuu wa Tshwane (ambayo una julikana kama Pretoria) pamoja na mji wa biashara wa Johannesburg.
Japo kuwa inasemekana bado mtandao huo utakuwa unafanya kazi kwa baadhi ya wateja waliochaguliwa, lakini msemaji wa kampuni ya Rain amesema kuwa kampuni hiyo inategemea kutanua upatikanaji wa huduma hiyo kwenye miji yote mikubwa ya nchini humo ifikapo mwaka 2020.
“Tumechagua baadhi ya wateja waliopo kwenye maeneo yaliyo na mtandao huo wa 5G kuwa wateja wa kwanza kununua data ya kasi ya 5G na kutumia bila ukomo kwa Randy R1,000 tu (sawa na TZS 155,000) kwa mwezi,” alisema Khaya Dlanga, afisa mkuu wa masoko wa kampuni ya Rain.
Mtandao huo ume tengenezwa na kampuni ya Rain kwa kushirikiana na kampuni ya Huawei ambapo inasemekana mtandao huo kwa sasa una kasi mara 10 zaidi ya mtandao wa 4G ambao unatumiwa na wateja wengi wa mtandao huo kwa sasa.
Dlanga alisema kasi ya MB 700 kwa sekunde katika hali bora ilirekodiwa wakati wa upimaji. “Walakini, katika hali halisi tunatarajia kuona angalau MB 200 kwa sekunde kwa wateja.”
Kampuni ya Rain inashirikiana na Chuo Kikuu cha Wits na Huawei Technologies kuanzisha Lab ya uvumbuzi wa 5G katika chuo kikuu cha Johannesburg. “Nafasi hii ya kupendeza itawapa wahandisi vijana mwanzo wa kukuza matumizi mapya ya ubunifu ya 5G” alisema Dlanga.