Wakati baadhi ya simu za Samsung zikiendelea kupata mfumo mpya wa Android 11 pamoja na mfumo wa One UI 3.0, hivi karibuni kampuni ya Samsung imetangaza kutoa mfumo mpya wa maboresho wa One UI 3.1 ambao utakuwa sambamba na mfumo wa Android 11.
Mfumo huo mpya wa One UI 3.1 ulitangazwa rasmi kupitia uzinduzi wa simu za Galaxy S21, na sasa mfumo huo upo tayari kuja kwenye simu nyingine za Samsung za daraja la juu pamoja na simu za daraja la kati.
Baadhi ya maboresho yanayokuja kwenye mfumo huo mpya wa One UI 3.1 ni pamoja na maboresho ya kamera ambapo sehemu mpya zimeongezwa kama vile sehemu mpya ambayo inaweza kurekodi video na kuchukua picha kwa wakati mmoja.
Sehemu nyingine inayoletwa na mfumo mpya wa One UI 3.1 ni pamoja na sehemu mpya ya kufuta sehemu au kitu ambacho huitaji kitokee kwenye picha zako mara baada ya kuchukua picha, kwa mujibu wa Samsung utaweza kufanya hivyo kwa kubofya mara moja tu.
Mbali na hayo, sehemu nyingine mpya kwenye mfumo huo ni pamoja na sehemu maalum ambayo itakusaidia kuweza kurekodi sauti kutoka kwenye vifaa vyako vyote kwa wakati mmoja yaani simu na simu nyingine, pamoja na simu na spika za Bluetooth za Samsung Buds Pro.
Sehemu nyingine ni pamoja na sehemu ya kuzuia mwanga wa simu usikuumize macho, sehemu hii itakusaidia kubadilisha aina ya mwanga unao tolewa na simu yako wakati wa mchana na wakati wa usiku ili kulinda zaidi macho yako.
Sehemu hizo na nyingine nyingi zinategemewa kuja hivi karibuni kwenye simu za Samsung za daraja la kwanza na daraja la kati, huku Samsung ikiwa imatangaza list ya simu za kwanza kupata mfumo huo ambayo nimekuwekea hapo chini.
- Galaxy S20 series zote
- Galaxy Note20 series zote
- Galaxy Z Flip 4G na 5G
- Galaxy Z Fold2
- Galaxy S10 series zote
- Galaxy Note10 series zote
- Galaxy Fold
- Galaxy A71
- Galaxy A51
- Galaxy A90
- Galaxy A80
- Galaxy A70
- Galaxy A50
Kwa sasa hiyo ndio list ambayo samsung imetangaza kupitia tovuti yake, kumbuka kuna uwezekano mkubwa wa list hii kuongezeka kwa siku za mbeleni hivyo endelea kutembelea ukurasa huu kujua list ya simu ambazo zitaongezwa hapo baadae.