Kama wewe uliwahi kutumia simu za Blackberry basi najua utakuwa unajua app ya kwanza ya kuchati ya BBM au BlackBerry Messenger, app hii ilikuwa maarufu sana kipindi hicho hadi hapo ilipo kuja app ya WhatsApp.
Kwa muda mrefu kampuni nzima ya Blackberry pamoja na huduma zake imekuwa ikitetereka hadi kufikia hatua ya kufunga baadhi ya huduma inazo miliki. Hivi karibuni kampuni hiyo imetangaza kusitisha huduma ya BBM au BlackBerry Messenger ambayo hii ni app inayopatikana kwenye soko la Play Store pamoja na kwenye simu za Blackberry.
Blackberry imetangaza kupitia blog yake kuwa, huduma hiyo itakuwa haipatikani kuanzia tarehe 31 ya mwezi wa tano kwa watumiaji wa kawaida wa app hiyo. Hata hivyo kama wewe ni mtumiaji wa App ya kulipia ya BBMe au BlackBerry Messenger Enterprise utaweza kuendelea kufurahia app hiyo kama kawaida. App ya BBMe sio app ya tofauti sana na BBM bali utofauti upo kwenye malipo ya dollar $2.50 ambayo hufanyika kila baada ya miezi sita.
Kampuni ya Blackberry kwa sasa ina tengenezewa simu zake na kampuni ya China ya TCL Corporation, kampuni ambayo kwa hapa Tanzania inasifika sana kwa kuuza TV za bei nafuu. Moja ya simu ambazo tayari ziko sokoni zilizotengenezwa na kampuni ya TCL kupitia Blackberry ni pamoja na simu za Blackberry Key2 pamoja na Blackberry KeyOne.
Kama wewe ni mpenzi wa BBM na ungetaka kuendelea kutumia BBM hata baada ya kufungwa nadhani ni wakati sasa wa kupakua app ya BBMe ambayo inabidi kulipia kiasi kidogo cha Tsh 6000 kila baada ya miezi sita. Unaweza kupata app ya BBMe hapo chini.