Hivi karibuni kampuni ya Sony iliandaa tamasha la uzinduzi wa PS5 mtandaoni ambalo lilikuwa lifanyike tarehe 4 mwezi Juni, lakini kwa bahati mbaya kutokana na maandamano yaliyokuwa yanaendelea nchini marekani kampuni ya Sony iliahirisha mkutano huo na kutangaza kuwa itatoa tarehe nyingine hapo baadae.
Hatimaye siku ya leo kampuni ya Sony kupitia akaunti ya Playstation ya Twitter, imetangaza kuwa kampuni hiyo inategemea kufanya tamasha lake la uzinduzi wa kifaa chake kipya cha Playstation 5 (PS5) hapo tarehe 11 mwezi juni, ikiwa ni siku mbili tu kutoka siku ya leo tarehe 9 mwezi juni.
Mpaka sasa tayari tunajua mambo machache kuhusu PS5, ikiwa pamoja na ujio wa controller mpya za kisasa, uwezo mpya wa uhifadhi wa SSD pamoja na muonekano mpya kabisa wa kifaa hicho kwa ujumla.
Mbali na hayo tunategemea kuona PS5 ikija na aina mpya ya teknolojia ambayo inafanya game za PS5 kuwa na muonekano bora na wakisasa kabisa ambao unakaribiana na muonekano wa filamu au movie. Unaweza kuangalia kipande kifupi cha game ambayo inasemekana ni ya PS5 hapo chini.
Kupata taarifa zaidi hakikisha unaendelea kutembelea tovuti ya Tanzania Tech kila siku kwani tutakuwa mubashara kabisa tukikuletea tamasha hilo litakalo kuwa likionyeshwa mtandaoni.