Kampuni ya kutoa huduma za simu ya Safaricom ya nchini Kenya, hivi karibuni imetangaza kupunguza viwango vya kutuma pesa kwa wateja wake kutokana na ugonjwa wa corona. Kwa mujibu wa tovuti ya CitizenTV ya Kenya, punguzo hilo litasaidia watumiaji wa Safaricom kutuma pesa bure chini ya kiwango cha Ksh 1,000 ambayo ni sawa na takribani Tsh 22,275.84.
Punguzo hilo linakuja baada ya Raisi wa Kenya, Uhuru Kenyatta, kutangaza kuwa kampuni za simu ziangalie njia za kuongeza matumizi ya pesa kupitia simu ili kupunguza maambukizi ya virusi vya corona ambayo yanaweza kutokea kutokana na msongamano wa watu.
“… shughuli zote za kutuma pesa kwa mtu mmoja kwenda mwingine chini ya Ksh1,000 zitakuwa bure. Hii inamaanisha kwamba, kuanzia leo asubuhi, tarehe 16 mwezi wa tatu, watumiaji wa M-PESA kupitia Safaricom wataweza kutuma kiasi chochote chini ya Ksh.1,000 bure kwa siku 90 (tisini) zijazo,” inasoma sehemu ya taarifa hiyo ya Safaricom.
Safaricom pia inafanya kazi na serikali kwa kutoa kituo cha kupiga simu na kuunganisha namba ya simu isiyo na malipo ambayo imewekwa na Kamati ya Dharura ya Kitaifa ya Kenya, ili kusaidia Wakenya katika kuelewa jinsi ya kuzuia na kusimamia kesi zinazoshukiwa za ugonjwa wa virusi vya corona. simu zote kwenda kwenye namba hiyo 719 zitakuwa bure.
Hadi kufikia siku ya leo tarehe 16 ya mwezi Machi mwaka huu 2020, kwa mujibu wa tovuti ya mwananchi tayari mgonjwa mmoja ametambulika kuwa na virusi vya corona nchini Tanzania.