Kampuni ya Simu ya Airtel Afrika pamoja na kampuni ya kuwezesha kutuma na kupokea pesa nje na ndani ya nchi ya Western Union, hivi karibuni zimetangaza ushirikiano wa pamoja ambao utawawezesha wateja wa Airtel Money kuweza kutuma na kupokea pesa kutoka nje ya nchi kwa kutumia huduma za Western Union.
Huduma hiyo itawaruhusu watumiaji kutuma na kupokea fedha kutoka akaunti zao za Western Union kwa kutumia akaunti zao za Airtel Money. Mbali na hayo wateja wa Airtel Money wataweza kutumia pesa hizo kulipa bili, kununua muda wa juu wa maongezi, na kutuma pesa ndani na nje ya nchi kwa urahisi.
Pia watumiaji wa huduma za Western Union kote duniani, wataweza kutuma pesa moja kwa moja kwenda kwenye akaunti ya mtumiaji wa huduma za Airtel Money kupitia huduma za kidigital za Western Union ambazo zinapatikana kwenye nchi zaidi ya 75, kupitia kwa mawakala zaidi ya 200 ambao wanapatikana kwenye nchi hizo.
Kwa sasa bado hakuna taarifa za lini huduma hii itanza kufanya kazi rasmi kwa hapa Tanzania, lakini kwa mujibu wa tovuti ya The Citizen Tanzania ni moja kati ya nchi zitakazopata huduma hiyo ikiwa pamoja na nchi nyingine za Afrika kama vile Nigeria, Uganda, Gabon, Zambia, DRC, Malawi, Madagascar, Kenya, Congo, Niger, Chad, Rwanda pamoja na Visiwa vya Shelisheli.
Airtel Tanzania itakuwa ni kampuni ya kwanza ya mawasiliano kwa hapa Tanzania, kuungana na Western Union kwa ajili ya kurahisisha kutuma na kupokea pesa kutoka nje ya nchi kwa gharama nafuu na kwa urahisi zaidi kwa kutumia simu za mkononi. Ili kujua jinsi ya kujiunga na huduma hii endelea kutembelea Tovuti ya Tanzania Tech kila siku tuta kuhabarisha zaidi.