Ni wazi kila mtu ambaye amewahi kutumia mtandao hasa hapa Tanzania ni lazima anafahamu angalu kidogo kuhusu kampuni ya Jumia, kama ufahamu sana kwa upande huo basi lazima utakuwa umeshawahi kuona au kutembelea tovuti za Jumia Tanzania ambazo hutoa huduma mbalimbali hapa Tanzania na nje ya Tanzania. Lakini pamoja na hayo, yapo mambo kadhaa ambayo huwenda ulikuwa huyajui kuhusu kampuni hii.
Kupitia makala hii ya Je wajua, nitaenda kukujuza angalau mambo machache ambayo nadhani ulikuwa huyajui hapo awali kuhusu kampuni ya Jumia. Basi bila kupoteza muda twende moja kwa moja tukangalie mambo haya.
TABLE OF CONTENTS
Jumia Market Ilikuwa ni Kaymu
Kaymu ilizinduliwa mwaka 2012 mwezi February na kwa kipindi hicho kaymu ilizinduliwa kwanza kwenye nchi za Nigeria pamoja na Pakistan na baadae kusambaa kwenye nchi zaidi ya 32 kwa muda wa mwaka mmoja. Mwaka 2016, Kaymu ilitangazwa kuwa inaunganishwa na bidhaa zingine za kampuni hiyo na zote kwa pamoja zitakuwa chini ya Jina moja la Jumia, hii ilifanya huduma zote zilizokuwa zinatolewa na Kaymu kipindi hicho kubadilika na kuwa na Jina la Jumia.
Jumia Imeanzishwa na Wazungu
Pamoja na kuwepo kwa mawazo kuwa Jumia ni kampuni ya kutoka Afrika, ripoti zinasema kuwa Jumia ni kampuni ya kizungu kutokana na kuanzishwa na wazungu. Kwa mujibu wa wikipedia, Jumia ilianzishwa na Jeremy Hodara na Sacha Poignonnec ambao hawa wote walikuwa wakifanya kazi pamoja kwenye kampuni ya usimamizi inayoitwa McKinsey & Company. Pia inasemekana kuwa wagunduzi wengine wa kampuni hiyo ni pamoja na Tunde Kehinde na Raphael Kofi Afaedor ambao hawa wote ni Waafrika.
MTN ndio Kampuni Yenye Hisa Nyingi Jumia
Kabla ya kampuni ya Jumia kuorodheshwa kwenye soko la hisa la marekani, Kampuni inayotoa huduma za simu ya MTN ya Afrika kusini ndio ilikuwa inaongoza kwa kumiliki hisa nyingi zaidi za kampuni ya Jumia. Kwa mujibu wa The Atlas, kampuni ya MTN ndio inaongoza kwa kuwa na share kwa aslimia 29.7% huku ikifuatiwa na kampuni ya Rocket Internet ya Ujerumani ambayo inamiliki asilimia 20.6 na nafasi ya tatu ikiwa ni kampuni ya Milicom ambayo ni kampuni mama ya Tigo ambayo yenyewe ina miliki asilimia 9.6. Hata hivyo Jeremy Hodara ambaye ni mwanzilishi wa Jumia ndio mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Rocket Internet ambayo ni ya pili kwa kumiliki share nyingi za kampuni hiyo baada ya MTN ya Afrika Kusini.
Jumia Ilianzishwa Tanzania Mwaka 2014
Kama nilivyo kwambia awali Jumia ilikuwa ikiitwa Kaymu na kwa hapa Tanzania, ilikuwa ikiitwa Kaymu Tanzania mnamo mwaka 2014, hadi hapo ilipo badilika na kuwa Jumia Tanzania. Mwanzo ilipokuja hapa Tanzania Kaymu ilikuwa ikifahamika zaidi kama mtandao wa kuuza na kununua ingawa ulikuwa ukitoa huduma zaidi ya hizo za kukutanisha wanunuzi na wauzaji. Kwa sasa Jumia Tanzania ni moja kati ya mtandao mkubwa unao fanya biashara mbalimbali za mtandaoni ikiwa pamoja na huduma za chakula, usafiri, huduma za malazi na huduma nyingine nyingi.
Jumia Soko la Hisa la Marekani Mwaka 2019
Mwezi Nne mwaka huu 2019, Jumia ikiwa kama kampuni ya kwanza ya kiteknolojia ya “kiafrika”, kwa mara ya kwanza ilifanikiwa kuingia kwenye soko la hisa la marekani maarufu kama (NYSE). Baada ya kuingia kwenye soko hilo, hisa za kampuni hiyo zilipanda kwa kasi hadi asilimia 75.6 na kufikia mtaji wa soko wa dollar za marekani Bilioni 3.9 ndani ya siku ya kwanza ya kuingia kwenye soko hilo. Hata hivyo inasemekana kuwa baada ya Jumia kuingia kwenye soko hilo, siku mbili baadae hisa za kampuni hiyo zilishuka hadi asilimia 40 baada ya kutokana na kile kilicho semekana kuwa ni taarifa za udanganyifu zilizokuwa zimechapishwa na tovuti maarufu ya Citron Research kuhusu kampuni ya Jumia.
Jumia Yasitishwa Nchini Tanzania
Kufikia tarehe 27 ya mwezi wa kumi na moja mwaka 2019, kampuni ya Jumia ilitangaza rasmi kusitisha biashara yake ya Jumia Market ambayo ilikuwa ikisaidia wauzaji na wanunuji kuweza kuuza bidhaa mbalimbali mtandaoni. Sababu za kusitishwa kwa Jumia Tanzania zilikuwa ni pamoja na kampuni hiyo kudai kuwa inataka kuangalia masoko mengine ambayo yatasaidia Jumia kukuwa zaidi.
Hata hivyo Jumia Tanzania ilifungwa siku chache baada ya kampuni hiyo kufunga biashara yake hiyo kwenye nchi ya Cameroon ambapo pia sababu zinasemekana kuwa hizo hizo za kuangalia masoko mengine yenye faida zaidi. Kwa sasa Jumia.co.tz imeelekezwa kwenye tovuti ya kuuza na kununua ambayo inafanana na tovuti maarufu ya kupatana.com.
Mengine Kuhusu Jumia
Na hayo ndio mambo machache ambayo huenda kulikuwa hujui kuhusu Jumia, Kama unataka kujua zaidi unaweza kusoma hapa kujua mambo mengine ambayo ulikuwa huyajui kuhusu kampuni ya Samsung, Kwa habari zaidi za je wajua hakikisha unaendelea kutembelea Tanzania Tech kila siku.