Kama wewe ni mfuatiliaji wa maswala haya ya teknolojia basi lazima unafahamu kuhusu simu mpya ya Huawei Mate 30, kama hufahamu hii ndio simu ya kwanza ya Huawei ambayo itaingia sokoni bila programu za muhimu kutoka Google, programu hizi ni pamoja na Play Store, Chrome, YouTube, Gmail, Google pamoja na apps nyingine mbalimbali ambazo zinamilikiwa na kampuni ya Google.
Kwa sasa bado hatujajua simu hiyo itakuja na programu gani ili kuisadia simu hiyo kufanya kazi kama simu nyingine za Android, lakini kitu kimoja ambacho tumefanikiwa kujua ni muonekano wa simu hizo mpya ambazo zinatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.
Kama unavyoweza kuona kwenye picha hapo juu, simu za Huawei Mate 30 na Mate 30 Pro zinatarajiwa kuja na mtindo mpya wa kamera ambapo sasa kamera zote za nyuma zitakuwa ndani ya duara maalum. Kamera hizo ambazo zitakuwa nne zinasemekana kuwa mbili zitakuwa na uwezo wa Megapixel 40, moja itakuwa na uwezo wa Megapixel 8, na moja ya mwisho itakuwa ni ToF camera.
Mbali na hayo Mate 30 Pro inasemekana kuja na kioo kikubwa ambacho kime tengenezwa kwa mtindo wa kisasa ambao unaitwa waterfall screen, mtindo ambao kioo cha simu hiyo kinakuwa na pembe zilizo jikunja sana kuanzia kushoto na kulia kama vile maporomoko ya maji au waterfall.
Kwa mbele simu zote mbili zinakuja na ukingo wa juu maarufu kama notch, ukingo ambao unatumika kuhifadhi kamera ya mbele pamoja na spika ya kusikiliza simu. Mate 30 yenyewe inaonekana kuja na ukingo mdogo kwa upana, wakati Mate 30 Pro inaonekana kuja na ukingo mkubwa kwa upana kutokana na kuwa na kamera tatu kwa mbele.
Kwa upande wa rangi Mate 30 Pro na Mate 30 zina onekana kuja kwa rangi za Black, Emerald Green, Space Silver pamoja na Cosmic Purple.
Kwa upande wa sifa inasemekana kuwa Mate 30 na Mate 30 Pro zote zinakuja na processor mpya za Huawei za Kirin 990, battery yenye uwezo wa 4,200 mAh kwa Mate 30 pamoja na 4,500 mAh kwa Mate 30 Pro. Simu hii ni moja akati ya simu za Huawei ambazo zinakuja na mtindo mpya wa Huawei wa EMUI 10 pamoja na mfumo mpya wa Android ambao hauna huduma za Google.
Simu hizi mpya za Huawei Mate 30 na Mate 30 Pro pamoja na Mate 30 Porsche zote zinatarajiwa kuzinduliwa hapo kesho tarehe 19 ya mwezi huu wa tisa, huko Munich nchini Ujerumani. Tutakuwa mubashaea tukikuletea uzinduzi huo hivyo endelea kutembelea Tanzania Tech.