Baada ya tetesi za muda mrefu hatimaye hivi leo kampuni ya Huawei imezindua rasmi mfumo wake mpya wa HarmonyOS, mfumo ambao mwanzoni ulikuwa ukijulikana kama HongmengOS.
Kupitia mkutano wa wabunifu wa kampuni hiyo, Huawei ilitangaza mfumo huo mpya wa HarmonyOS kama mfumo wenye uwezo wa kufanya kazi kwa haraka zaidi kwenye vifaa mbalimbali ikiwa pamoja na Smartphone, Smart TV, Smart Watch pamoja na radio za magari.
A modularized #HarmonyOS can be nested to adapt flexibly to any device to create a seamless cross-device experience. Developed via the distributed capability kit, it builds the foundation of a shared developer ecosystem #HDC2019 pic.twitter.com/2TD9cgtdG8
— Huawei Mobile (@HuaweiMobile) August 9, 2019
Kwa mujibu wa tovuti ya GSMArena, kupitia mkutano huo Richard Yu, ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa Huawei alisema kuwa, mfumo huo umekuwa ukitengenezwa na Huawei toka mwaka 2017 na unategemewa kuonekana kwa mara ya kwanza kwenye simu ya Honor, sehemu ya kampuni ya Huawei ambayo ndio inategemewa kuzinduliwa simu hiyo hapo kesho.
Hata hivyo mkurugenzi huyo alisema kuwa, kwa sasa bado kampuni ya Huawei itaendelea kutumia mfumo wa Android kama mfumo wa uendeshaji wa simu zake, lakini pia kama watumiaji wanataka kuhamia kwenye mfumo wa HarmonyOS watakuwa na uwezo wa kufanya hivyo kwa urahisi.
Kwa upande wa Apps watumiaji na wabunifu wataweza kuendelea kutumia Apps zote za Android kwenye mfumo huo wa HarmonyOS bila kikwazo chochote ikiwa pamoja na programu zote zilizo andikwa kwa kutumia lugha za kompyuta za HTML5 pamoja na Linux.
Kupitia mkutano huo Huawei imeanisha kuwa, lengo la mfumo huo mpya wa HarmonyOS ni kupita mfumo wa Android na kuwa mfumo bora na unaotumiwa zaidi duniani kuliko mfumo wa Android ulivyo hivi sasa.
Kwa sasa bado hakuna taarifa za zaidi kuhusu mfumo huo hivyo hakikisha unaendelea kutembelea Tanzania Tech kwani hapo kesho tutakuonyesha jinsi mfumo huo unavyo onekana kwenye simu hiyo mpya ya Honor.