Kama tunavyojua kampuni ya Google ndio inamiliki mfumo wa Android, katika kusherekea miaka 10 ya mfumo huo Google imatangaza kufanya mabadiliko ya majina ya mifumo ya Android ambayo awali ilikuwa na majina ya vyakula (dessert), mfano Android Pie, Android Nougat na mengine.
Kupitia tovuti yake Google imeainisha kuwa, kuanzia sasa majina ya Android hayato kuwa na majina ya ziada ya vyakula (dessert), na badala yake yatakuwa na namba pekee kama vile Android 10 ambayo awali ilikuwa ikijulikana kama Android Q. Google imeeleza kuwa mabadiliko hayo yamekuja baada ya kuona kuwa majina hayo yanalenga zaidi soko la marekani pekee ambapo majina hayo ya vyakula ndio yanatumiwa zaidi.
Google imesema, badala yake imeona ni bora kutumia majina ya namba ambayo yanalenga soko la duniani nzima ambapo mfumo huo wa Android unatumika zaidi kwa sasa. Kuanzia mfumo wa Android unaokuja baada ya Android 9 (Pie), mifumo yote ya Android itakuwa na majina ya namba pekee kwa mfano Android 10 na sio Android 10 Q.
Mbali na majina ya Android, Google pia imefanya mabadiliko ya Logo yake ya Android ambayo awali ilikuwa na muonekano wa kijani pekee, lakini sasa itakuwa na mchanganyiko wa rangi nyeusi pamoja na kijani ikiwa pamoja na kuongezewa picha ya roboti ya Android kwa mbele.
Kuanzia sasa logo ya Android pale utakapo kuwa unawasha simu mpya yenye Android kuanzia Android 10, itakuwa na picha ya roboti kwa mbele kama inavyoonekana kwenye picha hapo chini.
Google imesema kuwa, inategemea kuanza kutumia majina haya mapya pamoja na logo hiyo mpya ndani ya wiki chache zinazokuja pale mfumo wa Android 10 utakapo zinduliwa rasmi. Miongoni mwa simu zitakazo pata mfumo wa Android 10 wenye mabadiliko hayo, ni pamoja na simu ya TECNO Spark 3 Pro ambayo ndio itakuwa simu ya kwanza kutoka TECNO kupata mfumo huo mpya wa Android 10 ukiwa na logo hiyo mpya na majina hayo mapya.
Kupata habari zaidi kuhusu mabadiliko ya mfumo mpya wa Android hakikisha unaendelea kutembelea Tanzania Tech kila siku.