Google Yasitisha Baadhi ya Huduma Zake kwa Kampuni ya Huawei

Huawei haitoweza kutumia baadhi ya huduma zilizopo ndani ya mfumo wa Android
Google Yasitisha Baadhi ya Huduma Zake kwa Kampuni ya Huawei Google Yasitisha Baadhi ya Huduma Zake kwa Kampuni ya Huawei

Mzozo wa muda mrefu wa kampuni ya kielektroniki ya Huawei na serikali ya marekani umefikia kwenye sura mpya kwani hivi karibuni Google imatangaza kusitisha baadhi ya huduma zake kwa kampuni ya Huawei.

Ikumbukwe kuwa Google ndio mmiliki wa mfumo wa Android, masoko ya Play Store pamoja na huduma nyingine ambazo hutumiwa zaidi na watumiaji wote wa simu za Android.

Advertisement

Hata hivyo hatua hii inakuja wiki chache baada ya raisi wa marekani kutia saini makubaliano ambayo yanazitaka kampuni mbalimbali nchini humo, kupewa leseni maalum na serikali ili kuweza kuuza bidhaa zake kwa kampuni maalum za nchini China. Google ikiwa ni moja ya kampuni za nchini marekani inalazimika kufuata sheria hiyo na hivyo kufikia hatua ya kusitisha baadhi ya huduma zake kwa kampuni hiyo.

Huawei inaweza kuendelea kutumia mfumo wa Android ambao ni mfumo huru (Open Source), lakini haitoweza kutumia huduma za muhimu za Google ambazo mara nyingi zinaenda sambamba na mfumo huo ili kuweza kufanya mfumo huo kufanya kazi kwa usahihi.

Hata hivyo kwa mujibu wa Reuters, msemaji mmoja wa kampuni ya Google amethibitisha kuwa baadhi ya bidhaa za Google kama vile soko la Google Play na Google Play Protect, zitaendelea kufanya kazi kwenye simu za Huawei ambazo tayari zipo sokoni, Lakini hadi sasa haija julikana kama simu hizo zitaendelea kupata masasisho (update) mapya ya huduma za Google au simu hizo zitabaki kuwa na huduma za zamani za Google.

Vilevile bado haijajulikana hatua hii itaadhiri kwa kiasi gani watumiaji wa simu mpya na za zamani za Huawei, ila ni wazi kuwa lazima kutakuwa na usumbufu wa hapa na pale hasa kwenye simu mpya ambazo zinatarajiwa kuja au zilizotoka siku za karibuni.

Kampuni ya Huawei hivi karibuni imekuwa kwenye mgogoro mzito na Serikali ya marekani kwa kile kinacho semekana kwamba kampuni hiyo inaweza kutumiwa na serikali ya nchini China kusambaza vifaa vya kielektroniki vyenye uwezo wa kuchunguza Mitandao ya mawasiliano ya nchini Marekani.

Hata hivyo Huawei imekanusha madai hayo na kusema kuwa haiwezekani kwa Serikali ya China kutumia bidhaa zake kwa uchunguzi wa namna hiyo, huku ikidai kuwa hatua ya upingamzi wa bidhaa zake nchini marekani haitoweza kuzuia kampuni hiyo kukuwa kibiashara.

Huawei imetoa tamko kupitia barua pepe iliyotumwa kwa waandishi wa tovuti ya The Verge, barua hiyo haina majibu kamili bali maelezo yake yanazidi kuacha maswali zaidi kwa watumiaji wa simu za Huawei.

Sehemu ya barua hiyo imeandikwa, “Huawei imetoa mchango mkubwa katika maendeleo na ukuaji wa mfumo wa Android duniani kote. Kama mmoja wa washirika wa kimataifa muhimu wa Android, tumefanya kazi kwa karibu na jukwaa lao la wazi (Open Source) ili kuendeleza mazingira ambayo yamefaidisha watumiaji wote na sekta hiyo.

Huawei itaendelea kutoa sasisho za usalama na huduma za baada ya mauzo kwa watumiaji wa simu zote za Huawei zilizopo sokoni na zile ambao zinaendelea kutumiwa duniani kote. Huawei imesema, Tutaendelea kujenga mfumo wa programu salama na endelevu, ili kutoa uzoefu bora kwa watumiaji wa bidhaa zetu kote duniani. ”

Maelezo hayo bado yanaacha maswali mengi sana kwa watumiaji wa simu za Huawei za mfumo wa Android mara baada ya Google kutangaza kusitisha leseni na baadhi ya huduma zake kwa kampuni hiyo. Kampuni za Intel na Qualcomm nazo zimetangaza kusitisha biashara na kampuni ya Huawei kuanzia siku ya leo.

Kwa habari zaidi endelea kutembelea ukurasa huu kwani tutakuwa tunaongeza taarifa zaidi pindi tutakapo zipata rasmi.

Update 20-05-2019 : Makala hii imeongezwa kuonyesha Maelezo yaliyotolewa na kampuni ya Huawei.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

Pata Habari za Teknolojia Kupita Barua Pepe

By pressing the Subscribe button, you confirm that you have read and are agreeing to our Privacy Policy and Terms of Use