Kampuni ya TECNO imekuwa kimya kwa takribani miezi 3 toka ilipo zindua simu za Camon 11 na Camon 11 Pro November mwaka jana 2018, lakini hivi karibuni kimya hicho kinategemewa kuisha kwani kwa mujibu wa tetesi mbalimbali mtandaoni, kampuni hiyo inategemea kuzindua simu zake mpya za TECNO Spark 3 pamoja na TECNO Pouvoir 3.
TECNO sio kama kampuni nyingine ambazo hufanya siri muonekano wa simu zake mpya kwani hadi sasa tayari muonekano wa simu hizi unajulikana rasmi, huku pia baadhi ya sifa za simu hizo zote mbili zikiwa zinajulikana.
TABLE OF CONTENTS
TECNO Spark 3
Kama unavyoweza kuona kwenye tangazo la simu hii, TECNO Spark 3 inakuja na kioo cha inch 6.2 chenye ukingo wa juu pamoja na teknolojia ya IPS LCD display. Vile vile kwa mujibu wa tetesi inasemekana simu hizi zinakuja na resolution ya 720 x 1500 pixels. Kwa nyuma simu hii inasemekana kuja na kamera mbili za Megapixel 13 na Megapixel 2 ambazo pia zinakuja na teknolojia za AI au Artificial Intelligence.
Kwa upande wa processor TECNO Sparks 3 zote zinasemekana kuwa na processor moja ya Quad-core 1.3 GHz au 1.5 GHz ambayo inasaidiwa na RAM ya GB 2 pamoja na ukubwa wa ROM wa GB 16 au GB 32 kwa upande wa TECNO Sparks 3 Pro. Hadi sasa tofauti kubwa inayo julikana kati ya Spark 3 na Spark 3 Pro ni ukubwa wa ROM ambapo Spark 3 Pro inakuja na ROM ya GB 32 na Spark 3 yenyewe inakuja na ROM ya GB 16.
Mbali na hayo, TECNO Spark 3 na TECNO Spark 3 Pro zinategemewa kuwa ni maboresho zaidi kwenye upande wa kamera.
TECNO Pouvoir 3
Kwa upande wa TECNO Pouvoir 3 nayo pia inasemekana kuja na kioo cha inch 6.2 chenye teknolojia ya IPS LCD ambacho pia kina kuja na ukingo wa juu maarufu kama notch. Kama ilivyo TECNO Pouvoir 2, simu hii ya Pouvoir 3 yenyewe inaangalia zaidi battery kwani battery ya simu hii nayo inakuja na ukubwa wa battery ya 5000 mAh ambayo kwa mujibu wa TECNO idumu na chaji kwa muda wa siku nne au zaidi kulingana na matumizi yako.
Mbali na hayo TECNO Pouvoir 3 inasemekana kuja na kamera ya mbele ya Megapixel 13 yenye flash ya LED, Kwa nyuma simu hii inakuja pia na kamera ya Megapixel 13 ambayo inakuja na teknolojia ya AI au Artificial Intelligence.
Vilevile Pouvoir 3 inakuja na ukubwa wa ndani wa ROM wa GB 32 pamoja na RAM ya 2 au GB 3, huku ikiwa na teknolojia za ulinzi za kutambua uso (Face Unlock) pamoja na fingerprint iliyopo kwa nyuma. Mengine kwenye simu hii ni pamoja na radio FM pamoja na kutumia laini mbili.
Kwa sasa simu hizi bado hazijajulikana lini zitatoka rasmi, lakini kutokana na matangazo hayo huwenda simu hizi zikatoka rasmi mwezi huu, au mwanzoni mwa mwezi wa nne. Kwa habari zaidi kuhusu simu hizi pamoja na sifa zake kamili pamoja na bei hakikisha unaendelea kutembelea Tanzania Tech.