Kampuni ya Samsung bado inaendelea na ahadi ya kuangalia zaidi simu za daraja la kati, ahadi iliyotolewa hapo mwaka jana 2018 na mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Samsung DJ Koh.
Katika kuendeleza jitihada hizo, hivi karibuni tulisikia kuwa samsung inajiandaa kuja na simu mpya ya Galaxy A60 simu ambayo pengine itakuwa ni simu yenye sifa bora hadi sasa kwenye mfululizo mpya wa simu za Galaxy A.
Lakini kama haitoshi, hivi karibuni kumezuka tetesi mpya ambazo zinaelezea ujio wa simu mpya za Galaxy A20e, Galaxy A40 pamoja na Galaxy A90. Hadi sasa hakuna chochote kile ambacho kinajulikana kuhusu simu hizi bali ni majina tu ya simu hizo, hata hivyo kwa upande wa simu ya Galaxy A20e hii inasemekana kuwa ni simu ambayo huenda ikafanana kwa sifa na Galaxy A20.
Kwa mujibu wa tovuti ya GSMArena, majina ya simu hizi yameibuka baada ya tovuti ya Samsung ya nchini uingereza kuchapicha kurasa zinazo ashiria ujio wa simu hizo. Hata hivyo kwenye kurasa hizo ambazo hadi sasa zipo hewani, hakuna kitu chochote isipokuwa majina ya simu hizi kwenye kila kurasa.
Bado tunaendelea kufuatilia kuhusu ujio wa simu hizi hivyo hakikisha unaendelea kutembelea tovuti ya Tanzania Tech kwani tutakujuza yote yanayoendelea kuhusu simu hizi ikiwa pamoja na sifa zake kamili pamoja na bei pale zitakapo toka rasmi.