Ni wazi kuwa tumesha sikia mengi kuhusu Samsung Galaxy S10, Kama hii ni mara yako ya kwanza kusoma makala hii basi ngoja nikumbushe kidogo tetesi zilizopo hadi sasa kwa ufupi kabisa.
Kwanza inasemekana Galaxy S10 itakuwa na mtindo mpya wa kamera ambao tumeona kwenye simu mpya ya Samsung Galaxy A8s ambayo imetoka siku za karibuni. Pili inawezekana kuwa Galaxy S10 itakuwa na sehemu ya Fingerprint ambayo iko juu ya kioo, huku ikisaidiwa na teknolojia ya 3D kwenye fingerprint inayofanya sehemu hiyo kufanya kazi kwa haraka zaidi.
Tatu, Galaxy S10 Plus inategemewa kuwa simu kubwa zaidi, huku ikisemekana kuja na kamera mbili kwa mbele ambazo kamera hizi nazo zitakuwa juu ya kioo. Mbali ya yote pia Samsung inatarajia kufanya mabadiliko ya muonekano wa simu hizi kwa kuweka muonekano mpya wa One UI kwenye Galaxy S10, muonekano ambao utabadilisha kabisa icon na muonekano mzima wa simu hizo.
Yote haya na mengine mengi yanategemewa kufanyika siku ya tarehe 20 ya mwezi wa pili mwaka huu 2019 huko San Francisco nchini marekani. Kupitia mitandao mbalimbali, Samsung imetuma mialiko ya tamasha la uzinduzi wa simu yake hiyo, tamasha linalo tarajiwa kufanyika siku hiyo ikiwa ni jumatano saa (2) mbili usiku kwa saa za Afrika mashariki.
Bado mambo mengi sana yanatarajiwa kwenye uzinduzi huu, moja ya jambo kubwa linalo subiriwa pengine kuliko uzinduzi wa simu hizi ni uzinduzi wa simu ya kwanza ya Samsung inayo jikunja. Kama wewe ni mfuatiliaji wa Tanzania Tech lazima utakuwa umefanikiwa kuona muonekano wa simu hii japo kidogo ilipo onyeswa kwenye mkutano wa Samsung Developer Conference 2018.
Kama ulikuwa bize kidogo na huja fanikiwa kuona basi unaweza kusoma hapa utaweza kuona video ya simu hiyo ilipo onyeshwa kwa mara ya kwanza na Samsung. Mbali ya yote inasemekana kuwa simu hii ilionyeswa vizuri kwa watu wachache kwenye mkutano wa CES 2019 lakini mpaka sasa hakuna aliyetoa picha au muonekano halisi wa simu hiyo.
Haya yote na mengine mengi, tukutane mubashara kabisa kwenye tamasha hilo la uzinduzi wa simu hizo hapo tarehe 20 ya mwezi February.