Kampuni ya Xiaomi inajulikana kwa kutengeneza simu za bei nafuu ambazo zinakuja na teknolojia mpya, japokuwa kampuni ya Xiaomi haijulikani sana kwa kuwa na teknolojia mpya kwenye simu zake lakini pengine hilo linategemewa kubadilika siku za karibuni.
Hivi karibuni mwenyekiti mtendaji wa kampuni ya Xiaomi Lin Bin, ameonyesha aina mpya ya teknolojia ya fingerprint ambayo pengine itabadilisha kabisa jinsi tunavyo tumia teknolojia hiyo kwenye simu zetu.
Kupitia video fupi hapo chini utaweza kuona aina hiyo mpya ya fingerprint inayopatikana juu ya kioo ambayo ni tofauti kabisa na fingerprint nyingine za juu ya kioo unazo weza kuziona kwenye simu mbalimbali. Fingerprint hiyo mpya ya Xiaomi inauwezo wa kuwa kwenye kioo kizima, tofauti na kwenye simu nyingine ambapo ni lazima kushikilia sehemu husika ambayo huwa na alama maalum juu ya kioo.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, ukubwa wa eneo ambalo mtu anaweza kugusa ili kufungua simu yenye teknolojia hiyo ni Millimetre 50 kwa Millimetre 25, hii ikiwa ni sehemu kubwa zaidi kuliko sehemu ya kawaida ya fingerprint ambayo ni robo ya eneo hilo la fingerprint hiyo mpya ya juu ya kioo ya Xiaomi.
Mbali ya eneo la fingerprint hiyo kuwa kubwa, pia fingerprint hiyo inasemekana kufanya kazi kwa haraka zaidi kuliko hata fingerprint ya kawaida ambayo inapatikana kwenye simu mbalimbali za sasa, kama unavyoweza kuona kwenye video hapo juu mtu akifungua simu bila hata kuangalia.
Japokuwa teknolojia hii inaonekana kufanikiwa kwa kiwango kikubwa, lakini bado kuna maoni ya tofauti kuhusu teknolojia hii, moja ya maswali ambayo najua hata wewe unajiuliza ni kuwa inakuaje ukishika kwenye kioo kwa bahati mbaya tena ukizingatia teknolojia hiyo ufungua simu hata pale inapokuwa imezima kioo kabisa.
Hebu niambie nini maoni yako kwenye hili.?, ungependa kuona teknolojia hii ya fingerprint kwenye simu yako mpya utakayo nunua ? tuambie kwenye sehemu ya maoni hapo chini. Kwa sasa tuendelee kusubiri hadi hapo Xiaomi watakapo zindua simu ya kwanza yenye teknolojia hii, pengine tutaweza kujua ni jinsi gani teknolojia hii inavyofanya kazi.