WhatsApp ni moja kati ya programu zinazofanyiwa mabadiliko kila siku, mabadiliko haya huja kwanza kupitia programu za majaribio za WhatsApp Beta kabla ya kuwafikia watumiaji wengine ndio maana ni rahisi kwa baadhi ya sehemu mpya zinazokuja kujulikana na watu hata kabla ya kufika kwenye programu ya kawaida ya WhatsApp.
Wiki hii, moja ya mabadiliko ambayo yameweza kuonekana kwenye programu hiyo ni pamoja na njia mpya ya kuweza kuangalia picha na video kabla ya kuzifungua kupitia pazia la taarifa (Notification Panel) juu ya simu yako pale unapo pokea meseji mpya.
Kama inavyo onekana kwenye picha hapo juu, kupitia sehemu hiyo mpya utakuwa na uwezo wa kudownload picha au video moja kwa moja kupitia sehemu ya taarifa (Notification) na hivyo utaweza kuiangalia picha hiyo hata kabla ya kuifungua meseji yenyewe kupitia app ya WhatsApp.
Kwa mujibu wa tovuti ya WABetaInfo, sehemu hiyo ambayo sasa iko kwenye majaribio kupitia mfumo wa iOS, itafanya kazi iwapo utakuwa umewasha notification za aina ya Pop ambazo huonyesha meseji nzima pale ujumbe wa WhatsApp unapo ingia kwenye simu yako, hata hivyo pia watumiaji wa sehemu hii wataweza kudownload picha na video kupitia sehemu ya Notification iwapo sehemu ya kupakua picha na video imewashwa kupitia app ya WhatsApp.
Najua kwa upande mwingine sehemu hii sio rafiki sana kwa watumiaji wengi, kwani hii itafanya mtu kuweza kuona picha na video zako kupitia sehemu ya Notification kabla ya kufungua meseji yenyewe kupitia app ya WhatsApp.. Lakini pia kwa mujibu wa tovuti hiyo, kutakuwa na sehemu ya kuzima sehemu hiyo kama hutopenda kutumia.
Kwa sasa kama unataka kuzuia watu kuchungulia meseji zako, unaweza kufuata njia kwenye makala yetu iliyopita na utaweza kuzuia watu kusoma meseji zako za WhatsApp bila wewe kujua.