Matumizi ya mtandao yamezidi kukuwa sana siku hizi, lakini kuongezeka huku kwa matumizi ya mtandao kunachagiza kuibuka kwa sheria mpya za mtandao kwenye nchi mbalimbali ambazo sheria hizi kazi yake ni kudhibiti matumizi mabaya ya mitandao.
Siku za karibuni tumesikia sheria mpya mbalimbali za mitandao zikijitokeza kwenye nchi mbalimbali za Afrika ikiwa pamoja na sheria za kusajili bloggers iliyo anzia hapa Tanzania, pamoja na sheria ya kulipia matumizi ya mitandao ya kijamii iliyo anzia huko nchini Uganda, sheria hizi zote zimekuja baada ya kuonyesha kukuwa kwa kasi kwa matumizi ambayo sio sahihi ya mitandao mbalimbali.
Sasa habari kutoka mtandao wa Techweez zinasema kuwa hivi karibuni nchini zambia itapitishwa sheria mpya ya mtandao ambayo itawataka watumiaji wa mitandao kama bloggers na Group Admin wa mitandao kama Facebook na WhatsApp kupata kibali maalum kwa ajili ya kutumia mitandao hiyo.
Akizungumza kwenye mahojiano kupitia kituo cha kurusha matangazo cha ZNBC, Mkurugenzi wa Huduma za Usaidizi katika Mamlaka ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ya Zambia (ZICTA), Mofyta Chisala alisema, “Tunakuja na sheria ambazo sasa msimamizi anahitaji kusajiliwa ili aweze kuweka maadili au kanuni za maadili kwa mtu yeyote atakaye kuwa kwenye blogu hiyo kwa sababu mwishoni mwa siku, tutamkamata mtu huyo ambaye aliunda kundi la Whatsapp au mhariri au mratibu wa blogu na haitaishia hapo”
Kwa mujibu wa mtandao wa gs.statcounter, matumizi ya mtandao wa Facebook inchini zambia yana ongoza kwa asilimia 75.99% huku matumizi mengine makubwa yakiwa kwenye mitandao ya Youtube pamoja na Twitter.