Toleo jipya la mfumo wa uendeshaji wa kompyuta za Mac (macOS) sasa unakuja na jina jipya la macOS Mojave. Toleo hilo jipya limetangazwa jana kwenye mkutano wa WWDC 2018 na linakuja na mabadiliko mbalimbali ambayo kwenye makala hii tutapata nafasi ya kuangalia mabadiliko hayo mapya yanayo tarajiwa kuja kwenye mfumo huo mpya ambao utapatikana rasmi baadae mwaka huu 2018.
Basi bila kupoteza muda twende tukaangalie mabadiliko hayo.
Dark Mode
Kupitia toleo jipya la macOS Mojave, Apple imetangaza kuleta rasmi sehemu mpya ya Dark Mode, sehemu hii itakusaidia kuweka giza kwenye kompyuta yako na utaweza kutumia kompyuta yako bila kuona rangi nyeupe ambazo pengine zinaweza kuumiza macho yako hasa wakati wa usiku.
Muonekano wa Mac App Store
Apple pia imetangaza jana kuwa inabadilisha muonekano wa App Store kwenye kompyuta za Mac, na kwa mujibu wa Apple sasa muonekano huo utakuwa ni rahisi sana kutumia. Mbali na hayo Apple ilitangaza hapo jana kuwa inatarajia kuwa kampuni mbili kubwa zitaingiza rasmi programu zake kwenye soko hilo la programu la Mac App Store na kampuni zilizo tajwa ni Microsoft ambayo italeta Office 365 na Adobe ambayo inaleta Lightroom CC kwenye soko hilo la Mac App Store.
Desktop Stacks
Apple inaongeza njia mpya ya kusafisha desktops yako kupitia kipengele kipya cha “Desktop Stacks”. Kipengele hicho kitakuwa na uwezo wa kupanga mafolder yako juu ya desktop ya kompyuta na kuyaweka kwenye vikundi mbalimbali. Kwa mfano kama juu ya desktop yako kuna mafile ya PDF, images au movies, kupitia njia hiyo mpya ya “Desktop Stacks” utaweza kuona mafile hayo yakiwa yamekusanywa na kupagwa kulingana na aina ya mafile yaliyoko juu ya desktop yako.
Maboresho Zaidi ya Kivinjari cha Safari
Kupitia toleo hilo jipya la macOS Mojave, Apple inaongeza ulinzi zaidi kwenye mfumo wake mpya wa Mac na sasa itakuwa inakupa taarifa zaidi kuhusu tovuti zinazotumia Cookie kwa ajili ya kuchukua data zako kwa ajili ya mambo mbalimbali. Mbali na hayo kivinjari cha Safari kimeongezewa ulinzi zaidi na sasa kitakuwa kinazuia tovuti kama Facebook kweza kuchukua data zako.
Maboresho ya Sehemu ya Finder
Kupitia toleo jipya la macOS Mojave, Apple imeleta aina mpya ya kuangalia mafile au mafolder kupitia sehemu ya finder ambayo sasa utaweza kuangalia kwa kupitia njia mpya inayoitwa “Gallery”. Njia hii pia itakupa uwezo zaidi wa kuona mambo mbalimbali kuhusu file zako kwa urahisi zaidi.
Mabadiliko Mengine
Mabadiliko mengine ni pamoja na ujio wa aina mpya ya picha za kuweka kwenye desktop ambazo zitakuwa zinabadilika zenyewe kutokana na majira au saa, Vilevile toleo hili litakuja na njia nyingine rahisi ya kuweza kuchukua screenshot kwenye kompyuta yako.
Na hayo ndio baadhi ya mabadiliko yanayo tegemewa kwenye mfumo mpya wa macOS Mojave mfumo unao tegemewa kutoka rasmi baadae mwaka huu 2018. Bado mkutano wa WWDC 2018 unaendelea na hapa Tanzania tech tuna ukurasa maalum wa #WWDC 2018 ambapo unaweza kuendelea kupata habari zaidi kuhusu yote yanayoendelea kujiri kwenye mkutano huo.