Bado tupo kwenye mkutano wa F8 (2018) ulio anza kufanyika rasmi hapo siku ya jana, baada ya kuona kuhusu facebook kuja na sehemu mpya kukusaidia kupata mpenzi, sasa twende tukaangalie upande wa WhatsApp.
Programu ya WhatsApp inatarajiwa kufanyiwa maboresho kadhaa na moja kati ya maboresho hayo ni uwezo wa kikundi cha watu kuweza kupiga simu za video kwa kutumia programu ya WhatsApp. Kwa mujibu wa facebook, sehemu hiyo itawezesha hadi watu wanne kupiga simu za Video kwa pamoja kupitia sehemu hiyo mpya.
Mbali na hayo, maboresho mengine yanayo tarajiwa kufanyika ni pamoja na kuleta Stickers ndani ya programu za WhatsApp. Hapa utapewa uwezo wa kuchagua Sticker mbalimbali kama ilivyo kwenye programu za Facebook Messenger na nyingine kama hizo, Vilevile wabunifu wa programu watapewa uwezo wa kubuni programu za Sticker ambazo zitakuwa zinatumika na watumiaji wa programu za WhatsApp kutumiana Stickers mpya tofauti na zile zitakazo kuwa ndani ya programu ya WhatsApp.
Kwa upande wa programu ya WhatsApp kwaajili ya Biashara, watumiaji wataweza kuendelea kutumia programu hiyo bure kabisa, lakini kutakuwa na baadhi ya sehemu mpya ambazo mtumiaji wa programu hiyo atabidi kulipia ili kuweza kutumia sehemu hizo na kufikia wateja wengi zaidi.
Na hayo ndio maboresho machache yaliyo tangazwa hapo jana ambayo yanatarajiwa kufanyika kwenye programu za WhatsApp siku za karibuni. Mkutano wa F8 bado unaendelea kufanyika siku ya leo na kama tulivyo ahidi tutakuletea yote ya muhimu yatakayo jiri hivyo hakikisha unaendelea kutembelea Tanzania Tech ili kujua mengi zaidi.