Satelaiti ya kwanza kabisa iliyotengenezwa na wakenya inataraji kurushwa rasmi siku ya ijumaa ya wiki hii tarehe 11 mwezi wa tano mwaka 2018. Kwa mujibu wa tovuti ya The Star ya nchini Kenya, Kenya ina tarajia kuandika historia hiyo ya kurusha satelaiti hiyo huku tukio hilo likitegemewa kuonyeshwa mubashara na kituo cha televisheni cha KBC.
Hata hivyo kwa mujibu wa tovuti hiyo, Chuo Kikuu cha Nairobi kina waalika wananchi wote nchini humo kujumuika kwenye chuo hicho ili kuangalia tukio hilo mubashara kutoka nchini Japan ambapo ndipo satelaiti hiyo itarushwa kupitia huko kutokea kwenye stesheni ya anga ya kimataifa maarufu kama International Space Station (ISS).
ISS ni stesheni ya kimataifa ya anga iliyotengenezwa na mataifa mbalimbali, stesheni hiyo iko nje kidogo ya dunia ambapo ndipo Satelaiti hiyo ya Kenya ilipo kwa sasa. Satelaiti hiyo ilipelekwa huko siku ya Jumatatu ya tarehe 8 ya mwezi uliopita Aprili, ambapo ndipo itarushwa kutokea hapo na kuingia kwenye anga la ndani nje kabisa ya dunia.
Hata hivyo kwa mujibu wa makamu kiongozi wa chuo hicho kikuu cha Nairobi (UoN) Profesa Peter Mbithi alisema, Satelaiti hiyo imetengenezwa kwa gharama ya shilingi milion 120 za Kenya sawa na Shilingi za kitanzania bilioni 2.7 ambazo kwa kiasi kikubwa fedha hizo zilifadhiliwa kutoka nchini Japan. Kwa mujibu wa profesa huyo wahandisi kutoka chuo cha Nairobi walisaidiwa na wataalamu kutoka Shirika la Utafutaji wa Anga la Japani (Jaxa) kutengeneza Satelaiti hiyo.
“Hichi ni kitu cha kwanza cha nje ya anga kilichosajiliwa na Kenya na pia ni Satelaiti ya kwanza ya Kenya ambayo itaingia kwenye mzunguko wa anga,” Prof Mbithi alisema siku ya Jumatatu.
Hata hivyo Satelaiti hiyo inakuja kwenye muundo unaojulikana kama (nanosatellite) ambapo satelaiti hizi huwa ndogo sawa na mche mraba wa 10×10 wenye uwezo wa ujazo wa lita moja. Satelaiti hizi zinauwezo wa kufanya kazi mbalimbali ambazo hapo awali zilikuwa zikifanywa na satelaiti kubwa.
Tofauti na Satelaiti kubwa satelaiti za muundo huu wa (nanosatellite), hazirushwi kutoka duniani bali hizi hupelekwa kwenye stesheni ya anga ya kimataifa (ISS) ndipo baadae hurushwa kutokea hapo. Profesa Mwangi Mbuthia, ambae ni kiongozi wa shule ya wahandisi ya chuo hicho kikuu cha Nairobi alisema, shule hiyo ndio kitakuwa na sehemu maalum ya kuendeshea satelaiti hiyo.
“Satellite hii ina maisha ya kati ya mwaka mmoja hadi miezi 18, baada ya hapo itaondoka kwenye mzunguko wa angana na kuungua,” alisema Profesa Mwangi Mbuthia.
Hata hivyo kwa mujibu wa Profesa huyo satelaiti hiyo imetangenezwa na kamera pamoja na kinasa sauti ambacho kina uwezo wa kuchukua sauti na kuzituma moja kwa moja mtandaoni, Alisema satelaiti hiyo ina uwezo wa kufanya mambo mbalimbali ikiwa pamoja na kufanya kazi ya kuwezesha kuchukua ramani ya duniani, kuchunguza anga pamoja na kazi nyingine nyingi.
Satelaiti hiyo ilitengenezwa kwa njia ya mpango unaojulikana kama KiboCUBE, uliozinduliwa mnamo Septemba 2015, na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Mambo ya Nje ya Anga, United Nations Office for Outer Space Affairs au (UNOOSA) pamoja na Japan Aerospace Exploration Agency (Jaxa).