Vodacom Tanzania Yatisha Huduma za Kununua Umeme za Luku

Vodacoma imesema bado mazungumzo yanaendelea kurudisha huduma hiyo
Vodacom Tanzania Yatisha Huduma za Kununua Umeme za Luku Vodacom Tanzania Yatisha Huduma za Kununua Umeme za Luku

Habari kutoka kwenye gazeti la kila siku la mwananchi siku ya leo zinasema kuwa, Kutokana na kutokidhi masharti ya mfumo wa malipo serikalini (GePG), Vodacom imesitisha huduma za malipo ya Luku kwa wateja wake wa M-Pesa.

Mkurugenzi wa mawasiliano wa Vodacom, Rosalynn Mworia amesema wanaendelea na mazungumzo na Serikali kupata muafaka kabla ya kurejesha huduma hiyo. “Huduma ya Luku imesitishwa mpaka makubaliano na Serikali yatakapokamilika. Tunachukua juhudi za makusudi kuhakikisha muafaka unapatikana na huduma kurejea kama kawaida,” alisema Mworia.

Mfumo mpya wa ununuzi wa Luku ulianza kutumika Aprili 2 na wateja wanaotumia huduma za Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wanatakiwa kuufuata ili kuendelea kupata huduma. Meneja wa Uhusiano wa Tanesco, Leila Muhaji alisema jana kwamba baada ya kuanza kutumika kwa mfumo huo, uhusiano kati ya shirika hilo na wauzaji wengine wa umeme umekoma.

Advertisement

Alisema kuanzia sasa, mkataba wa kuuza nishati hiyo unafanywa baina ya wakala na Serikali. “Zamani mawakala wote walikuwa wanapitia Tanesco lakini sasa wanatakiwa kujiunga na mfumo wa Serikali. Baadhi wamekamilisha utaratibu wengine wanaendelea kukamilisha,” alisema Leila.

Hata hivyo, alisema wateja wanaotumia mita za Luku wataendelea kupata huduma kutoka ofisi za shirika hilo, maduka ya Tanesco na vituo vya mafuta, mawakala wa Selcom na Maxcom na benki za CRDB na NMB. Kwa wateja wanaotumia simu za mkononi alisema mpaka sasa, kampuni za Tigo, TTCL na Airtel ndizo zilizokamilisha utaratibu na kukidhi vigezo vya kuendelea kutoa huduma hiyo.

Updated 4/4/2018 Saa 5:20 PM – Ripoti kutoka kwenye tovuti ya Swahili Times zinasema, Vodacom wametoa tamko na kusema kuwa itaendelea kutoa huduma za umeme kama kawaida lakini Kutakuwa na ongezeko la asilimia moja nukta moja ya gharama halisi (1.1%) anayotozwa mteja ili kununua umeme pindi atumiapo huduma ya M-Pesa.

Licha ya Vodacom, Leila aliitaja mitandao mingine ambayo ipo kwenye hatua za kujiunga kwenye mfumo huo kuwa ni Halotel na Zantel. “Maboresho yanaendelea kutatua changamoto kadhaa zilizojitokeza. Tutaendelea kuwajulisha namna bora ya kupata huduma za Luku,” alisema Leila.

Kwa upande wa Halotel Meneja mawasiliano wa Halotel, Mhina Semwenda alisema majadiliano na Serikali yamekamilika na kuanzia leo watakuwa wameunganishwa kwenye mfumo mpya. “Kuanzia saa sita usiku leo (jana) Halopesa watakuwa wanajiunga kwenye mfumo wa Serikali. Majaribio yatafanywa muda huo kwa sababu kunakuwa na wateja wachache na baada ya hapo huduma itaendelea kutolewa kama kawaida,” alisema Semwenda.

Miongoni mwa mabadiliko yaliyoletwa na mfumo mpya ni kupungua kwa kamisheni iliyokuwa inalipwa kwa mawakala wanaohudumia wateja mtaani. Hata hivyo, taarifa ambazo hazikuthibitishwa zinadai kwamba asilimia za malipo kwa mawakala zitapungua chini ya mfumo huo mpya.

Mkuu wa kitengo cha masoko na ubunifu wa kampuni ya Maxmalipo, Deogratius Mosha alikiri kuwapo kwa mabadiliko ya malipo bila kubainisha kiasi akisisitiza kuwa taarifa hizo ni siri baina yao na mawakala na si jambo la kuweka wazi kwa vyombo vya habari. “Ninachoweza kusema ni kuwa huduma zetu zinaendelea kama kawaida licha ya mabadiliko madogo yaliyojitokeza.

Tayari tumeunganishwa kwenye mfumo wa Serikali. Siwezi kulisemea suala la malipo kwa kuwa kila wakala ana uhuru wa kuendelea na biashara au kujiondoa,” alisema Mosha. Mmoja wa mawakala wa Maximalipo jijini Dar es Salaam, Martha Joseph alisema alipata ujumbe kutoka Maximalipo kuwa kutakuwa na mabadiliko ya kimfumo kuanzia Aprili 2 lakini huduma zitaendelea kama kawaida na malipo yake hayatabadilika.

Kutokana na ujumbe huo, alisema aliwasiliana na ofisa anayemhudumia kupata ufafanuzi zaidi ambaye alimhakikishia kuwa huduma zitaendelea kama kawaida lakini kutakuwa na mabadiliko ya malipo yatakayopungua kidogo. “Sijapata ujumbe maalumu lakini huyo kaka aliniambia kuwa malipo yatapungua. Zilipoondolewa faini za polisi katika huduma za Maxmalipo, faida ilipungua sijajua hili nalo litakuwa na athari kiasi gani katika biashara,” alisema Martha.

Habari Hii Imenakiliwa Kutoka Gazeti la Mwananchi.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

Pata Habari za Teknolojia Kupita Barua Pepe

By pressing the Subscribe button, you confirm that you have read and are agreeing to our Privacy Policy and Terms of Use