Hivi karibuni kampuni ya Facebook kupitia mtandao wake wa facebook imeingia kwenye kashfa kubwa ya kuvujisha data za watumiaji wa mtandao huo kupitia kampuni ya Cambridge Analytica. Kashfa hiyo inaendela kuchukua sura mpya kila siku na leo mambo yamezidi kuwa magumu zaidi huku aliyekuwa mwanzilishi muandamizi wa App ya WhatsApp ambayo sasa ina milikiwa na Facebook akichangia kwenye kampeni inayosema ni wakati wa kufuta na kuachana na mtandao huo wa Facebook.
Brian Acton ambaye aligundua app ya whatsapp pamoja na mwenzake Jan Koum, aliyasema hayo jana kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter, huku akitumia hashtag ya #deletefacebook alionzishwa kwa kushinikiza watu kutaka mtandao huo kufutwa. Facebook ilinunua whatsapp mwaka 2014 kwa dollar za marekani bilioni $19 na wagunduzi hao wawili waliendelea kufanyia kazi programu ya Whatsapp wakiwa kama sehemu ya kampuni ya Facebook hadi pale Brian Action alipo amua kujiuzulu na kuachana na Facebook mapema mwaka huu.
Kitendo hichi cha Brian kushiriki kwenye kampeni hii, kimezua maswali mengi huku watu wakijiuliza kama mwazilishi huyo aliondoka vizuri kwenye kampuni ya facebook au kulikuwa kuna ugomvi baina ya mwazilishi huyo na kampuni hiyo. Kuhusu mwenzake ambaye alikuwa mwanzilishi mkuu wa WhatsApp Jan Koum, yeye bado anafanyia kazi mtandao WhatsApp akiwa chini ya kampuni ya Facebook.
Kwa sasa bado sakata la mtandao wa Facebook na kampuni ya Cambridge Analytica linaendelea huku kiongozi wa mtandao huo akihitajika kutoa majibu mbele ya viongozi wa seneti ya Marekani.