Hivi karibuni programu ya WhatsApp inaonekana kuongezewa vipengele vingi zaidi na vyenye kuboresha matumizi ya programu hiyo, katika kusisitiza hilo hivi karibuni WhatsApp imeanza kutoa toleo jipya la programu hiyo likiwa na aina mpya ya status ambayo ipo tofauti na ile iliyozoeleka.
Aina hiyo mpya ya Status ni ya kipekee kwani sasa mtumiaji ataweza kuweka video fupi inayo fanana na ile ya kwenye Instagram stories kama status kwenye programu hiyo. Vile vile kama ilivyo kwenye programu ya Snapchat video hiyo haito dumu kwa muda mrefu kama tulivyozoea kwenye status za kawaida za whatsapp, bali hivi sasa statu hiyo ya video itapotea kila baada ya masaa 24 yani siku moja baada ya kuiweka.
Akiongea na waandishi wa tovuti ya teknolojia ya Gadgets 360 ya india meneje bidhaa wa WhatsApp alisema kuwa aina hiyo mpya ya status ni mchanganyiko wa sehemu tatu ambazo tayari zilikuwepo kwenye programu hiyo, sehemu hizo ni broadcast lists, media sharing, pamoja na sehemu ya kawaida ya status ambayo ndio inatumika sana kwa sasa.
Ili kutumia sehemu hiyo mpya itakubidi kuangalia sehemu mpya ambayo ipo katikati ya sehemu ya Chats na Calls ambapo hapo utaona sehemu hiyo ambayo kupitia hapo utaweza kutengeneza status yako kama ilivyo kwenye Snapchat au Instagram Stories. Hata hivyo ndani ya sehemu hiyo ya kuweka status pia utaona status zako ambazo ulisha wahi kutengeneza pamoja na status zile ambazo marafiki zako walitengeneza ndani ya masaa 24 yani siku moja.
Sehemu hiyo mpya imesha tolewa rasmi na sasa imeanza kusambaa kwenye nchi za Europe na inategemewa kusambaa kwa watumiaji wote wa programu za WhatsaApp za Android, iPhone na Windows dunia nzima.